Wakaazi wa Mombasa watakiwa kujihusisha kikamilifu kwenye masuala ya ardhi

Wito umetolewa kwa wananchi wa kaunti ya Mombasa kujihusisha kikamilifu katika masuala ya ardhi.Akizungumza na vyombo vya habari katika mkutano na wadau, afisa anayesimamia masuala ya ardhi katika shirika la HAKI YETU John Polo Bonyo amesema kuwa kati ya watu 50 katika kaunti ya Mombasa, 2 ndio wanaojua nambari za ardhi yao.

Bonyo amesema kuwa hali hiyo ndiyo inayowapa mabwenyenye fursa ya kunyakua ardhi kwa urahisi kwenye kaunti ya Mombasa.

Kauli hiyo imeregelewa na mwenyekiti  wa wakaazi wa Tudor Estate katika kaunti ya Mombasa Samuel Chalo ambaye ameeleza kuwa watu wachache kwenye kaunti hiyo wana hatimiliki za ardhi zao.

Mkutano huo vilevile umejadili suala la ubora wa nyumba kwenye vitongoji duni kwenye kaunti ndogo ya Mvita, msimamizi wa kaunti hiyo ndogo Salim Kingi akieleza kuwa ipo haja ya kupunguza msongamano wa watu kwenye vitongoji duni kwa kujenga nyumba bora za kisasa.

Kingi kwa ushirikiano na shirika la HAKI YETU wamechagua watu kutoka kila wadi eneo bunge la Mvita watakaosaidia kukusanya habari kuhusu mradi wa kujenga nyumba zitakazowafaa  watu wote na baadaye kupeleka mapendekezo hayo kwa wasimamizi wa kaunti ya Mombasa na waziri wa ardhi wa kaunti hiyo ili kuzifanyia kazi.

Aidha,wadau mbalimbali waliohudhuria kikao hicho wametaka serikali kuu kutekeleza kikamilifu ripoti ya Ndung’u kuhusu ardhi na ardhi ya umma itwaliwe kutoka mikono ya mabwenyenye.

Pia,wametaka mfumo wa kutupa maji taka kwenye mitaa katika kaunti ya Mombasa iimarishwe kwani wajenzi wa kibinafsi wanaojenga nyumba kwenye mitaa hukosa kujenga tangi za Septik za kuhifadhi maji taka.

Wanasema kuwa hali hiyo inachangia kuharibiwa kwa mazingira kwenye vitongoji duni na maeneo hayo kuwa hatari kiafya.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *