Kenya yaadhimisha siku ya kimataifa ya viti vya magurudumu

Kenya imejiunga na nchi zingine kuadhimisha siku ya kiti cha magurudumu hafla hilo ikiandaliwa mjini Mombasa katika karakana ya Bombolulu kauli mbiu ikiwa kiti changu cha magurudumu haki yangu kujumuishwa.

Wadau mbalimbali wamejitokeza kwenye hafla hiyo naibu mwenyekiti wa bodi ya muungano wa watu wenye ulemavu APDK Bright Oywaya  akieleza umuhimu wa viti vya magurudumu ikiwemo kuwapa uhuru wa kufika hospitalini kwa matibabu,kufika shuleni na kwenye ofisi za serikali kupokea huduma miongoni mwa maeneo mengine. Vilevile viti hivyo huwapa msukumo na motisha wa kwenda nje kujitafutia riziki ya kila siku.

Bi Oywaya ameimiminia sifa siku hiyo akisema inawapa fursa ya kuwashukuru watu wanaopatiana na kutengeneza viti vya magurudumu kama APDK pamoja na kujikumbusha kuwa kuna mamilioni ya watu waliotaka kuwa na viti hivyo lakini hawakujaliwa wakati ambapo takwimu kutoka umoja wa mataifa inasema kuwa watu milioni mia moja wanahitaji viti vya magurudumu.

Aidha,Oywaya ametoa wito kwa serikali kupunguza ushuru kwa bidhaa wanazotumia kutengenezea viti vya magurudumu, viti hivyo vijumuishwe kwenye mpango wa serikali kuu wa kutoa huduma bora za afya (Universal Healthcare) na marekebisho yanayopangiwa kufanyiwa mswada wa watu wanaoishi na ulemavu nchini ukamilike na upitishwe na bunge.

Abdulaziz Shekue mwenyekiti wa timu ya wachezaji wa tenisi wakitumia viti vya magurudumu hakuficha furaha yake akielezea umuhimu wa viti hivyo kwenye mchezo wao.

Shekue ameeleza kuwa mchezo huo umewafanya kuzuru mataifa ya nje ikiwemo Tanzania,Uholanzi,Afrika kusini na Italia pamoja na kupata fedha za kujikimu baada ya kushiriki kwenye mashindano hayo.

Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto zimekuwepo ikiwemo bei ghali za kupata viti za magurudumu  na kukosa uwanja maalum wa kufanyia mazoezi yao.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *