Hotuba ya Maraga kuhusu utendakazi wa idara ya Mahakama yagubikwa na malalamishi

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga akiwa kwenye hafla ya kutoa ripoti kuhusu utendazaki wa idara ya Mahakama wa Mwaka wa 2019/2020 Picha kwa hisani ya David Maraga Kutoka Twiteer

Hotuba ya jaji mkuu nchini David Maraga inayotathmini utendakazi wa Idara ya Mahakama katika mwaka wa 2019/2020 Ijumaa Novemba 27, 2020 iligubikwa na lawama kwa rais Uhuru Kenyatta.


Tofauti za wawili hao zilijitokeza punde Maraga akigusia hatua ya Rais Kenyatta kutowateua majaji 41 (mmoja aliaga dunia) walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama JSC akisema hatua hiyo imelemaza utendakazi wa Mahakama.


Maraga aliongezea kuwa kibinafsi hana ila na rais Kenyatta na kwamba amempa heshima kama kiongozi wa nchi.


“Ni bayana kuwa kuna tofauti za kimaoni kati yetu lakini nikuhakikishie sina chochote kibaya dhidi yako. Mimi si mwanasiasa wala sina nia ya kuingia siasa kwa hivyo mbona nikupige vita?”akasema Jaji mkuu.

Mrundiko wa Kesi kortini ni mojawapo ya changamoto kwenye idara ya mahakama, akisisitiza kwamba alipochukua hatamu za uongozi kulikuwa na kesi 170,186 zilizokuwa na miaka mitano na zaidi kortini lakini mwisho wa mwezi Juni ,2020 waliweza kusikiza na kuamua kesi 201,206 .


Aidha hadi Juni 30, 2020 ni Kesi 35,359 pekee zenye zaidi ya miaka tano kortini ndizo hazijaamuliwa.

Vilevile idadi ya majaji katika mahakama ya rufaa imechangia ongezeko la mrundiko wa kesi kortini , Maraga akisema mahakama ya rufaa ina majaji 16 tofauti na majaji 30 wanaohitajika kushughulikia kesi hizo.


“Mrundiko wa kesi zaidi ya mwaka mmoja kortini (kwenye mahakama ya rufaa) umeongezeka kutoka 3,681 mwaka wa 2018/2019 hadi 4,982 mwaka wa 2019/2020,” ripoti inanukuu.

Jaji mkuu aidha alieleza kuwa idara ya Mahakama ina mchakato wa kuunda mahakama itakayoshugulikia kesi ndogo ndogo yenye chini ya dhamana ya milioni moja ili kuhakikisha kesi hizo zimesuluhishwa haraka.


Maendeleo pia yaligusiwa kwenye ripoti hiyo, Maraga akisema korti 61 zaendelea kujengwa , 21 kati yao zikiwa zimefadhiliwa na benki kuu ya Dunia , zilizobaki zikifadhiliwa na serikali kuu ya Kenya.


Serikali za kaunti na wabunge kupitia hazina ya maendeleo kwenye maeneo bunge (CDF) zilipongezwa kwa kusaidia katika ujenzi wa korti kote nchini.

Suala la kupunguza bajeti ya idara ya mahakama kutoka bilioni 2.1 hadi milioni 50 lilijirudia Maraga akiitaka serikali kuu kutoa kati ya shilingi bilioni 5 na 10 kwa idara ya mahakama kuisaidia kwa maendeleo.


Maraga anatarajiwa kustaafu mwezi ujao Desemba, Naibu wake Philomena Mwilu akishikilia wadhifa huo mchakato wa kutafuta jaji mkuu mpya ukiendelea.

About Author

Leave a Reply to Anonymous Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *