Shughuli ya kukusanya sahihi za BBI yazinduliwa

Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga Kwenye shughuli ya kuzindua ukusanyaji wa sahihi za BBI Picha kwa hisani ya Twitter/Raila Odinga
Shughuli ya kukusanya sahihi kuunga mkono ripoti ya Jopo la maridhiano BBI imezinduliwa rasmi Jumatano ya Novemba 25, 2020 na rais Uhuru Kenyatta pamoja na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali nchini Kenya.
Raila Odinga amewarai wakenya kujitokeza na kupiga sahihi , akisema ni ukurasa mpya Kenya inafungua.
Odinga amesema ripoti hiyo inawapa Wakenya wote fursa sawa kutimiza ndoto zao.
Amepuzilia mbali madai kuwa ripoti hiyo inaleta Rais atakayekuwa na mamlaka makubwa , akisema amekuwa mwathiriwa wa uongozi mbaya.
Vilevile , Odinga ametetea vipenge kwenye ripoti hiyo inayotaka vyama vya siasa kuteua makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya IEBC, akisema mbinu hiyo ilisaidia kuanda uchaguzi huru mwaka wa 2002.
“Tukubali uchaguzi uliokuwa huru (nchini Kenya) ni ule wa 2002 ulioongozwa na tume ya uchaguzi yenye makamishna walioteuliwa na vyama ….nchi nyingi zinatumia mfumo huo kwa maana vyama vya siasa ndio wahusika,” alisema Odinga.
Rais Uhuru Kenyatta kwa upande wake amesifia ripoti ya BBI akisema itawapa wanawake nafasi bora ya kujihusisha kwenye uongozi , walemavu kupata uwakilishi madhubuti bungeni , pesa kwa wadi kwa minajili ya maendeleo na seneti kupewa nguvu ya kufanya serikali za kaunti kuwajibika.
Rais amesema salamu za heri ‘Handsheki’ kati yake na Raila Odinga imeleta amani nchini humo kwani Kenya ilikuwa kwenye mgawanyiko ambao ungelemaza maendeleo.
“Pasingekuwa na salamu za heri nchi hii ingekuwa pabaya. Handsheki imefanya nchii hii kuwa imara na kutupa fursa ya kuimarisha umoja wetu, usawa na uongozi bora,” alisema Rais Uhuru Kenyatta.
Amesema ripoti ya BBI iliwapa wakenya fursa ya kutoa maoni yao na kutoa mapendekezo yatakayo saidia kusuluhisha shida za Kenya.
Aidha, Rais Kenyatta amesema huu ni wakati mzuri wa demokrasia na mabadiliko ya katiba yanahitajika.
Kiongozi wa nchi ametoa wito shughuli hiyo ya kukusanya sahihi ifanywe kwa kuzingatia sheria za wizara ya Afya za kudhibiti msambao wa virusi vya corona.
Shughuli ya kukusanya sahihi inatarajiwa kukamilika baada ya wiki moja.