Rais Uhuru kenyatta na naibu wake William Ruto wabainisha kuwa uhusiano wao haujadhoofika

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wamebainisha wazi kuwa bado uhusiano wao uko dhabiti baada ya habari kutokea kuwa uhusiano wao ulikuwa umedhoofika.


Tangu rais Kenyatta kutoa hotuba yenye hisia kali iliyoonekana kumlenga Ruto ,wawili hao walijumuika pamoja kwa mara ya kwanza kwenye hafla ya kufungua upya kiwanda cha Rivatex kilichoko kaunti ya Uasin Gishu, eneo bunge la Kapseret.


Mkutano huo haukuonyesha dalili ya watu waliokosana ila hotuba zao zilijawa na mipango ya kuhudumia wakenya kimaendeleo.


“Wewe ndiye kiongozi wetu wa taifa la Kenya na tuko nyuma yako, mbele na nyuma, kulia na kushoto kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” Ruto alimuarifu rais.


Viongozi hao walikiri kuwa mgawanyiko hauna nafasi tena katika serikali ya sasa kwani safari waliyoanza mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu ni ya kuunganisha wakenya.


“Kila wakati ninaendelea kuhimiza na kusisitiza jambo moja kwamba wakenya tuwe kitu kimoja tushirikiane kwa pamoja,” Rais alisema.


Ruto aliongezea kuwa serikali ya Jubilee inatambua walipoanzia na malengo yao mawili makuu ni kuwaunganisha wakenya wote pamoja bila ubaguzi wowote na kubadilisha mfumo wa kisiasa uwe ule mfumo wa kimaendeleo.


Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alimkumbusha rais kuwa Ruto ndiye aliyesimama naye kwa muda mrefu na hivyo asimsahau miaka ijayo.Alimahidi rais kuwa raia na viongozi kutoka kaunti ya Uasin Gishu watamuunga mkono kwa vyovyote vile maanake hapo mbeleni watahitaji mkono wake pia.


Rais Kenyatta aliwarai wafanyikazi wa humu nchini kuvalia mavazi yanayotengenezwa na viwanda vya humu nchini ili kupiga jeki ufanisi wa ajenda ya viwanda.


Kiwanda cha Rivatex kilisitisha shughuli zake miaka kumi iliyopita baada ya mali yake kuporwa lakini serikali ya Kenya ikishirikiana na serikali ya India zilitoa shilingi billioni mbili kukifufua.

Imeandikwa na kipkemoi Lang’at

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *