Waziri Magoha awatahadharisha wezi wa mitihani ya kitaifa

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha (Picha Kwa Hisani)
Waziri wa elimu Profesa George Magoha amewatahadharisha wanafunzi,wazazi na wakenya kwa jumla dhidi ya wizi wa mtihani wa kitaifa ya KCPE na ile ya KCSE, akihakikisha kuwa hilo halitafanyika huku akidhibitisha mitihani hiyo ipo kwenye kontena chini ya ulinzi mkali.
Akizungumza na vyombo vya habari katika shule ya msingi ya Sparky mjini Mombasa, Magoha amewahakikishia wanafunzi kuwa shughuli za mtihani zitaendelea kama ilivyopangwa na wanafunzi wote waliojisajili kwa mtihani huo wataikalia hata wale watahiniwa wajawazito.
“kila mwanafunzi atafanya mitihani hiyo mahali alipojisajili isipokuwa wale kutoka shule za kibinafsi ambazo zilifungwa na wakalazimika kuhamia shule nyingine,”akasema Magoha.
Magoha pia amewatahadharisha maafisa kutoka wizara yake dhidi ya kuwahamisha wanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine kwa sababu ya mitihani ya kitaifa.
Waziri huyo ameelezea imani yake kuwa yale ambayo wanafunzi hao wamefunzwa darasani yamewatosha kufanya mitihani ya kitaifa akiwataka wasitie hofu.
Vilevile,waziri Magoha amewashukuru wazazi na walimu kwa kuhakikisha usalama wa kiafya wa wanafunzi wakati huu wa janga la corona.