Watanzania bila cheti cha Korona kuwekwa karantini ya lazima Kenya

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo (Picha Kwa Hisani)

Kamati ya dharura inayoshughulikia janga la korona katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya imetoa masharti na mapendekezo yatakayosaidia kudhibiti msambao wa korona ikizingatiwa taifa liko katika wimbi la tatu la maambukizi.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kamishna wa kaunti ya Mombasa na mwenyekiti wa kamati hiyo Gilbert Kitiyo amesema Mikutano ya siasa itaendelea kuwa marufuku kwa siku thelathini huku wakipendekeza kutekelezwa kwa sharti ya kukaa umbali wa mita moja unusu kwenye treni ya SGR na safari za usiku za ndege na SGR kusitishwa ikizingatiwa zinakwaruzana na amri ya kutotoka nje .

Wakaazi wanaotumia feri watatakiwa kutumia kivuko cha liwatoni kupunguza msongamano huku wasafiri kutoka Tanzania na nchi za kigeni wasiokuwa na vyeti vya kuonyesha hawana Korona kuwekwa karantini ya lazima wanapoingia nchini.

“Maeneo ya biashara na kampuni za kutengeneza bidha za kusafirishwa nje ya nchi (EPZ)  yatakaguliwa na maafisa kutoka wizara ya afya ili kuhakikisha wameafikiana na kanuni za kudhibiti virusi hivyo,” akaongeza Kitiyo.

Aidha  maeneo ya kuabudu,shule na vyuo vikuu yametakiwa  kuhakikisha wanafuata kanuni za kudhibiti msambao wa virusi hivyo  huku wasafiri kutokaTanzania na nchi za kigeni wasiokuwa na vyeti vya kuonyesha hawana Korona kuwekwa karantini ya lazima.

Kitio pia ametoa hakikisho kuwa kamati hiyo itahamasisha umma na maafisa wa afya kuhusu umuhimu wa kuchanjwa.

Kwa upande wake Gavana wa Mombasa Hassan Joho ameeleza kufadhaishwa kwake na mapuuza ya wananchi kwa kutozingatia kanuni za kudhibiti Korona akiwataka kutokiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kwani hakuna atakaye sazwa na sheria.

“Wananchi waelewe korona bado ipo na hakuna mtu maalum kuliko mwengine. Kama una jengo sharti ufuate kanuni za kudhibiti msambao wa korona,” akasema Joho.

Joho ameongeza kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wa korona hufika hospitalini tayari wakiwa kwenye hali mahututi hivyo basi kuwekwa kwenye ventileta.

Vilevile, amedokeza kuwa watafunguwa upya maeneo ya kujitenga wagonjwa wa wakorona .

Takwimu kutoka serikali ya kaunti ya Mombasa zaonyesha kuna vitanda 100 vya kuhudumia wagonjwa wa korona. Aidha, wahudumu wa afya takribani 800 na maafisa 5 wa polisi  kutoka kaunti hiyo wamechanjwa.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *