Balozi wa Uingereza nchini ataka wanawake kuungana dhidi ya dhulma za jinsia

Bi Sadia(Kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa balozi wa Uingereza nchini Bi Jane Marriot Picha kwa Hisani Kutoka Twita

Huku Ulimwengu ukisherehekea siku ya kimataifa ya Wanawake ,Wanawake katika kaunti ya Mombasa wamehimizwa kushirikiana kupiga vita dhulma za jinsia.

Akiongoza Kinamama hao kwenye ukumbi wa Tononoka hapa Mombasa ,Balozi wa Uingereza humu nchini Jane Marriot amesema mwanamke mmoja kati ya watatu wameathirika na dhulma hizo.

Kulingana naye visa hivyo vimeongezeka zaidi wakati wa ujio wa virusi vya korona nchini huku akiwataka wanawake kuonyesha maadili mema katika jamii ili kupigana vita dhidi ya visa hivyo.

“Kujiita mwanamke haitoshi tu, yafaa tuonyeshe maadili na uongozi,” akasema balozi Marriot.

Marriot amenena hayo baada ya kuzindua nambari ya kupiga simu(0800720587)  na ya ujumbe mfupi (21094) ambapo wanawake watapiga ripoti na kupata usaidizi pindi wanapoathirika na dhulma za jinsia.

Mradi huo umeasisiwa na shirika la Sauti ya Wanawake Pwani na REINVENT kupitia kwa msaada wa serikali ya Uingereza.

Balozi huyo ameshukuru mashirika ya kina mama kama Sauti ya mama Pwani miongoni mwa mashirika mengine kwa juhudi zao za kuunga mkono kina mama na kueneza kampeni dhidi ya dhulma za jinsia.

Wakati huo huo Marriot amedokeza kuwa Uingereza imejitolea kikamilifu kukabiliana na dhulma za jinsia akieleza kuwa Kenya imekuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo.

Aidha amedokeza kwamba Uingereza imekuwa muhisani mkubwa ulimwenguni tangu 2013, kwa kutoa msaada wa pauni milioni 43 katika vita dhidi ya ukeketaji na wana mipango ya kuweka mikakati zaidi ya kupigana na vita hivyo.

Kilele cha hafla hiyo imekuwa Bi Sadia Hussein kupokezwa tuzo ya Commonwealth Points of Light kutoka malkia wa Uingereza kwa juhudi zake katika kampeni dhidi ya ukeketaji wa wasichana katika jamii yake.

Akiongea baada ya kupokea tuzo hiyo, Bi Sadia ameeleza furaha yake akieleza kuwa hata rudi nyuma katika safari yake ya kukomesha ukeketaji wa wasichana nchini.

“ Ukeketaji umetunyang’anya amani na furaha yetu.Nitahakikisha tumepambana na dhulma hiyo na kukomesha kitendo hicho,” akasema Bi Sadia.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *