Wanawake wahimizwa kujihusisha katika biashara

Bi Saadia Abdi akihutubia wanawake waliohudhuria hafla hiyo (Picha Kwa Hisani)

‘Kuwa mchapakazi, mwenye kujituma, mtu anayeomba na mwenye uwazi ndizo nguzo muhimu endapo wataka kuwa mwanamke mfanyabiashara mwenye mafanikio,’ ndio kauli ya Bi. Saadia Abdi mfanyabiashara na mwasisi wa kampuni ya SAA events inayopanga na kuwezesha hafla zinazosaidia jamii.

Bi. Abdi alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa SwahiliPot Jumamosi ya Machi 6, 2021 kwenye hafla iliyowaleta pamoja wafanyabiashara wanawake kutoka Kaunti ya Mombasa nchini Kenya. Wafanyabiashara hao walipata fursa ya kutangamana na wenzao, kubadilishana mawazo na kujikuza kibiashara.

Mfanyabiashara huyo alisema wanawake wanaweza kujitegemea ikizingatiwa wana talanta licha ya jamii  kuwadhalilisha kwa muda mrefu.

“Wanatuona kama watu wa kuketi nyumbani na kuzaa.Tuna talanta, uwezo na tunaweza kujitegemea,”akasema Bi Abdi.

Aliendelea kwa kuhimiza wanawake kuanzisha biashara za mapishi na urembo kwani soko lake ni kubwa na liko tayari.

Kauli za Bi. Saadia Abdi zilirejelewa na mfanyabiashara mwenza Bi Zahra wa kampuni ya SUP KENYA inayotangaza biashara kupitia ukurasa wao wa kijamii wa Instagram na kutumia mapato hayo kuwekeza katika uhisani.

Zahra alisifia hafla hiyo akisema imempa nafasi ya kukutana na wafanyabiashara na kujifunza mengi kutoka kwao.

“Nimekutana na biashara nyingi sikujua zilikuwepo mwanzoni. Najua wakumwendea nikihitaji kitu Fulani,”akasema Zahra.

Ahimiza wanawake kuanzisha biashara zinazoziba pengo fulani wakitaka biashara zake zifanikiwe.

“Nilianzisha biashara ya Nyali Play House iliyowapa watoto nafasi ya kucheza, niliwapa nafasi ambayo haikuwepo Mombasa. Hata baada ya janga la korona, biashara bado inanawiri,” akasema Zuhura.

Bi. Fathiah Omar, ambaye ni mwandishi wa habari na mfanyabiashara aliyehudhuria hafla hiyo na kusema kwamba hafla hiyo ilimpa fursa ya kueleza changamoto anazozipitia na namna ya kusaidiana kwa madhumuni ya kustawi  katika biashara.

Aliwataka wanawake kujitokeza kwani mazingira ya kibiashara inafunguka kwa wanawake licha ya kuwa sekta imetawaliwa na wanaume.

Vilevile, aliwasihi wanawake kuwa wavumilivu na kutofanya ukahaba ili kupata kazi au nafasi za biashara na badala yake kutafuta wahisani watakaowasaidia.

“Mafanikio hayaji kwa haraka. Nguzo ya maendeleo ni elimu. Kama nyumbani hakuna wa kukusaidia basi kuna mashirika ya kutetea haki za wanawake kwa hivyo wasijiuze, wawaendee,” akasema Bi Omar.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *