Ukraine yaomba usaidizi wa ndege za kivita

Ukraine President Zelenskyy Image credits (Ukrainian Presidential Press Office via AP)

Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wamekuwa na mkutano mjini Brussels kwa ahadi ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine “bila kuchoka” ikiwa ni pamoja na uwezekano wakuipatia nchi hiyo ndege za kivita.

Mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya umemalizika baada ya Saa 16 za majadiliano makali juu ya suala la Ukraine. Mkutano huo umetoka na kauli moja kuu ya kuendelea kulisaidia taifa hili lililo vitani na kuahidi kufanya inavyowezekana kuiwezesha kuzishinda hujuma za Urusi.

Mkutano huo umetiwa ari zaidi na uwepo wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ambaye amefanya ziara mjini Brussels kuzungumzia moja kwa moja mahitaji ya Ukraine mbele ya viongozi wa Ulaya.

Viongozi wa mataifa haya wamesema katu hawataitupia mkono Ukraine hadi ishinde vita dhidi ya Urusi, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema haondoi uwezekano wa kuipatia Ukraine ndege za kivita kama ilivyoombwa na rais Zelenskyy.

Suala la Ukraine kupewa ndege za kivita ilikuwa ajenda ya wazi ya rais Zelenskyy alipofanya ziara ya siku tatu barani Ulaya. Aliiweka mezani alipokuwa mjini London, akalitaja tena alipokutana na rais Macron na chansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Paris.

Akiwa mjini Brussels Zelenskyy alimwomba moja kwa moja mkuu wa Slovakia Eduard Heger ndege za kivita za enzi ya Muungano wa Kisovieti aina ya MiG chapa 29 ombi ambalo Heger alijibu atalifanyia kazi.

Mbali na suala la ndege ambalo baadhi ya viongozi wamesema ni pendekezo litakalochukua muda mrefu kuafikiwa,mkutano huo umekubaliana kutazama uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa silaha za kivita kwa ajili ya Ukraine kuanzia mwezi ujao kama msaada wa haraka.

Rais wa baraza kuu la umoja wa Ulaya Charles Michel amesema kanda hiyo itafaa ifanye kazi na sekta ya viwanda kuhakikisha kasi ya kutengeneza risasi na mabomu inaongezwa kutimiza mahitaji yaliyopo Ukraine. Pia, walichukua hatua ya kutumia euro bilioni 67 kusaidia kijeshi na kifedha Ukraine ikiwemo fedha zilizotumika kuwapokea wakimbizi milioni 4 kutoka Ukraine.

Ukraine wanahitaji madege ya kisasa kabisa ya kivita kutoka nchi za magharibi kwa sababu jeshi lao linakabiliwa na mashambulizi mapya ya Urusi.

Mzozo kati ya Urusi na Ukraine ulianza Februari 2014, ukihusisha vikosi vya wanaotaka kujitenga vinavyosaidiwa na Urusi kwa upande mmoja na Ukraine kwa upande wa pili. Mzozo huu unahusu hasa hadhi ya Crimea na Donbas.

About Author

1 thought on “Ukraine yaomba usaidizi wa ndege za kivita

Leave a Reply to Brian Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *