Ukabila Hautupeleki Mahali Ng’o!

Huku taifa likielekea katika awamu ya uchaguzi,kuna mjadala huwa haukwepi kwenye midomo ya watu. Kila pembe ya nchi,suala la ukabila hugusiwa si majumbani,kwenye mikutano ya kisiasa,shuleni hata mitandaoni jambo hili huzungumziwa.

Cha kusikitisha miaka nenda miaka rudi donda hili sugu hujirudia. Inaonekana hapajapatikana dawa mujarabu wa kumaliza ugonjwa huu,lakini leo nahisi imefika wakati tujadili suala hili kwa mapana na tulizike kwenye kaburi la sahau.

Hatuhitaji kukumbushana yaliyojiri mwaka 2007/2008 pindi tu matokeo ya uchaguzi  yalipotangazwa. Huhitaji kuelezwa namna familia zilivyotenganishwa,uhusiano baina ya jamii kusambaratishana,namna jamii hii lilivyofurusha jamii nyingine kutoka eneo lao.

Hakuna furaha kuelezea namna biashara zilivyoathirika na familia kupoteza pato. Sihitaji kukujuza namna uchumi wan chi yetu ulivyoharibiwa kisa na maana ghasia ziliibuka kiini kikiwa tofauti za kikabila.

Hivi kuna nini kikibubwa kwenye ukabila katika mipaka ya Kenya inayotutenganisha kiasi hichi? Nilidhani wito wa Harambe na Nyayo chini ya rais Jomo Kenyatta na Daniel Moi ulipaswa kutuleta pamoja.

Kizazi kipya kilitoa nafasi murua kama taifa kupunguza makali ya ukabila lakini jinsi mambo yanavyoenda bado tuko mbali katika harakati za kuangamiza jinamizi hili.

Ipo haja ya kukubaliana kwa pamoja jinamizi hili linaturudisha nyuma kisiasa,kisosholojia na kiuchumi.Kwa kifupi tuseme ukabila hautupeleki mahali ng’o.

Yapaswa tuanzishe mjadala huu upya mara hii tuwakandamize wanaoendesha kampeni za kuwatenganisha wakenya kwa misingi ya kikabila. Wa kwanza tunaopaswa kuwalenga ni wanasiasa na viongozi kwa jumla.

Aghalabu hao huwa mstari wa mbele kwa kutoa matamshi ya chuki. Maneno yanayodhalilisha jamii moja na kuipa sifa nyingine. Yapaswa tuwakomeshe.Tusiwakaribishe mitaani mwetu iwapo ajenda yao kubwa ni kutugawanya. Redioni na kwenye televisheni wasikubaliwe kwenye vipindi kutoa cheche za matusi na vilevile kwenye magazeti wasinukuliwe.

Pili, ni sisi wakenya. Masikini hoehae.Wepesi wa kudanganywa.Sisi ambao tunapopatiwa shilingi 50 tuko radhi kuanzisha vita dhidi ya wenzetu wa kabila lingine.

Yafaa tuwe na kikao. Tuzungumze kwa mapana. Tuelezane kwa kina.Tuambiane ukweli,ukweli ukiwa sisi ni mandugu,sisi ni wamoja kitu kimoja,dhehebu moja,Mungu mmoja na kuwa ukabila ni kitu kidogo na hakipaswi kututenganisha.   

Mwandishi mmoja ananukuliwa “Utofauti wetu haufai kututenganisha ila unapaswa kutufanya tugundue uhitaji wa kila mmoja wetu.” Yasikitisha kuona kuwa wakenya maskini ndio hutumiwa kuendesha gumzo la chuki baina ya jamii.

Inafedhehesha zaidi ninapong’amua maskini ndio huatharika pakubwa na hizo ghasia.Wanakosa pato wakati matajiri waliofadhili ghasia wanatumia fursa hiyo kuongeza bei za bidhaa mujimu na huduma.

Haitubainikii hata kidogo kuwa sisi ndio hubaki omba omba mitaani na kulazimika kurudi vijijini kwa kuwa gharama ya maisha imekuwa zaidi kiasi cha kutushinda kuimudu.

Hivi nitakuelezaje Otieno na Atieno ni mandugu? Kiprono na Cheprono ni umbu? Hivi nikuelezeje Nafula na Wafula ni wa jamii moja? Nitumie lafudhi gani ili nikushawishi kuwa makabila yetu  hayafai kuwa misingi ya kutugawanya bali kutuleta pamoja.

Hebu tafakari tunapoleta pamoja juhudi za kina Aisha wapwani wenye mchango mkubwa katika sekta ya utalii kwa ueledi wa mapishi. Unganisha mchango wa kina kamau katika sekta ya biashara na mauzo.

Changanya na historia ya jamii ya wamaasai kupitia mavazi yao ya kitamaduni inayovutia watalii kutoka kote ulimwenguni.Jumlisha na nguvu za waluhya na wajaluo wakiwa kifua mbele kwenye ukulima.
Ushawaza tukiungana twaweza tekeleza mengi kama taifa.

Nilipendeza sana na Rais wa taifa la Tanzania hayati Dkt John Pombe Magufuli katika siku zake za uhai alivyopenda kuwaunganisha watanzania kwa kuwahutubia kwa lugha azizi ya Kiswahili kila mara kiasi cha wafulani kumdhania kuwa hakujua kuzungumza Kingereza.

Aidha, napendezwa mno na jinsi Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kabarange Nyerere alivyoyaunganisha makabila zaidi ya mia moja na ishirini ya Tanzania na kuwa na lugha moja ya kuwaunganisha; lugha ya Kiswahili.

Nikimnukuu mzee katika mojawapo ya hotuba yake, “Katika karne ya ishirini na moja tupande basi la makabila, huo ni ujinga na upumbavu. Watanzania mnataka kutambika?” 


Hebu tafakari uzito wa maneneo hayo na mchango wa Nyerere katika kuwaunganisha watanzania, mlinganishe na Rais Uhuru Kenyatta anayezungumza lugha ya mama katika mikutano ya kitaifa ilivyoshuhudiwa miezi chache iliyopita katika ikulu ndogo ya Sagana.


ni ombi langu kuwa tujizatiti kupigana na “Ndwele” hii hatari hasa tunapokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022. Tuepukane na siasa chafu za kikabila, tusibaguane katika msingi huu wa kikabila.

Tuwachague viongozi wetu kwa msingi wa utendakazi na upendo kwa taifa lao. Natazamia siku ambayo Kiprono , Otieno, Wafula, Mutua, Mwangi, Ekuwam… wataitana ndugu na kupendana kama wakenya. Natazamia siku ambayo Wakenya tutaunganishwa kwa lugha moja. Umoja ndio nguvu yetu.


Imeandikwa na Mzalendo kindakindaki Kongowea Alex Barasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *