Tukitaka tajriba kazini tuandae mabaraza ya chifu badala ya mihandara vyuoni

Ninaweza kuapa kwamba kamati mbalimbali za shule, hospitali, mashirika ya kiserikali kwa jamii, hazina ya eneobunge almaarufu CDF na viwanda vya miwa, kahawa na majani kule vijijini zimejaa walimu, madaktari, polisi na wafanyakazi wengine wengi wa serikali waliostaafu.

Nakiri kwamba kazi hizo zinahitaji ujuzi au tajriba toshelezi sababu zinahusiana na mpango mzima wa kuendesha shirika husika kifedha na kadhalika. Lakini iwapo tunaimania sana katika wazee wastaafu na tajriba zao, mbona tunawapeleka vijana vyuoni? Si afadhali kuandaa vikao vya baraza la chifu ili wazee waliostaafu wafundishe vijana hawa namna ya kupata tajriba?

Tunaishi katika nchi ambamo rais ni mtoto wa rais, wakili ni mtoto wa wakili, hakimu ni mtoto wa hakimu vilevile meneja na kadhalika. Hata seneta pia ni mtoto wa seneta na mbunge akiaga anarithiwa na mwanawe aliyesomea ughaibuni?

Hili linadhihirisha wazi kuwa tajriba inaweza ikarithishwa kutoka kizazi hadi kingine. Kila ninapowazia hali hii najikuta nikiradidi swali moja, je, mtoto wa maskini atawai kuwa tajiri? Nani atamrithisha maskini tajriba wanayotaka waajiri kazini iwapo kijana huyu ndiye wa kwaza kuwahi kufika chuo kikuu katika familia yake ya kimasikini?

Ninahisi kuwa nafasi za ajira humu nchini zinaweza zikazidi idadi ya vijana. Tatizo lililopo ni kwamba wazee wastaafu wamekalia nyadhifa nyingi wanazomiliki kwa madai kuwa wana tajriba. Wengi wa wazee wenyewe huwa mara wanakamati mara wasimamizi wa mashirika zaidi ya moja wanakofakamia marupurupu kama punje za wali.

Mathalan kule kijijini utamkuta mzee aliyekuwa daktari zamani ndiye mwanakamati wa almashauri ya shule tatu za upili. Mzee huyo huyo tena ndiye mwenyekiti wa kiwanda cha kahawa za wakulima na kwa wakati mmoja ni mwanakamati wa hazina ya eneobunge. Mzee wa aina hiyo atakosaje kumpigania mwanawe aliyesomea astashahada ya kilimo awe ndiye meneja wa akaunti ya hazina ya eneobunge?

Tena mzee huyo atakosaje fanaka katika kumpigania mwanawe apewe zabuni ya kusambaza bidhaa katika shule hizo tatu? Hata kama wajukuu wa mzee mwenyewe wanasomea ulaya, yeye atasikilizwa tu kama kwamba ni mzazi wa hapo.

Vijana wanapolia kila kuchao kuhusu ukosefu wa ajira, serikali inaonekana kuwajazia nta masikioni. Vijana wana haki ya kuandamana, kulalamika na kudai serikali nafasi za ajira. Wananchi ni sehemu ya serikali hata ingawa viongozi fulani wanaonekana kukana hilo paruwanja katika vituo vya habari.

Kwani demokrasia ni nini? ‘Simba’ Geofrey Mung’ou mwandishi na mtangazaji wa Radio Maisha anaonekana kupinga kuwa nchini hamna demokrasia, eti kuna domokrasia na tumbokrasia . Alipata.

Aggrey Barasa

About Author

2 thoughts on “Tukitaka tajriba kazini tuandae mabaraza ya chifu badala ya mihandara vyuoni

  1. My spouse and I absolutely love your blog and find almost all of your post’s to be precisely what I’m looking for. Does one offer guest writers to write content for you personally? I wouldn’t mind composing a post or elaborating on a lot of the subjects you write related to here. Again, awesome web site!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *