Rais Samia Suluhu awaongoza watanzania kumpigia kwaheri Hayati rais Magufuli

Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Kwenye ikulu Dar es Salaam (Picha Kwa Hisani)
Rais wa Tanzania Bi Samia Suluhu ameongoza watanzania kutoa pole zao za mwisho mjini Dodoma kwa hayati rais Dkt John Pombe Magufuli.
Kwenye hafla iliyohudhuriwa na marais kutoka nchi mbalimbali akiwemo rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Bi Suluhu amemmiminia sifa kedekede mtangulizi wake.
Amemtaja rais Magufuli kama mtu jasiri, mchapakazi, mtiifu, mwana mageuzi,mchapakazi,mzalendo na mwana mwema wa afrika aliyejenga uchumi wa Tanzania,kuzima ufisadi na kuwekeza kwenye miradi.
Suluhu amesema rais Magufuli aligusa mioyo za watu kwa muda mfupi alipokuwa madarakani kwa kuwa aliweka nchi mbele hali hiyo ikidhihirika na maelfu ya watu watu waliojitokeza kumuomboleza.
Kibinafsi rais Samia Suluhu ameeleza kuvutiwa na namna Hayati rais alivyotoa michango yake bungeni na kwenye baraza la mawaziri.
“Niliona dhamira ya mtu anayependa kazi yake. Alizijua barabara zote za nchi hii,urefu,majina na fedha zilizotumika kuzijenga,” akasema Rais Suluhu.
“Hakuogopa kukitetea kile alichoamini ni sahihi kwa maslahi ya taifa hata kama kingehatarisha nafasi yake,” akaongezea rais Suluhu.
Vilevile,amempongeza Hayati rais Magufuli kwa kuinua nafasi ya kina mama kwa kumteua kuwa naibu wake.
Hata hivyo rais Samia Suluhu amewasuta vikali wanaotilia shaka uongozi wake kwa misingi ya yeye kuwa mwanamke.
“Kwa wale wanashaka kuwa mwanamke huyu atawezana kuwa rais wa Tanzania,nataka niwaambie anayesimama hapa ni rais. Niko tayari kuendeleza kazi ya Hayati rais Magufuli,”akasema Rais Suluhu.
Kwa upande wake, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemtaja Hayati rais Magufuli kama mtu mchapakazi aliyeonyesha kuwa nchi za Afrika zaweza kujitoa kutegemea nchi za kigeni huku akitaja kifo chake kuwa pigo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.