Nzige ambao wamekuwa tishio kubwa katika taifa sasa wamekutana na pwaguzi. Wadudu hao ambao wamekuwa wakiogopwa na jamii nyingine nchini sasa wanaonjeshwa vikaangio huko magharibi.

Wakaazi wa kaunti za Bungoma na Trans nzoia wamepokelea uvamizi wa nzige hao kwa msisimko na bashasha. Picha nyingi mitandaoni zinaonesha nzige waliokaushwa wakianikwa wazi wazi kama nafaka huko vijijini. Picha nyingine zinaonesha nzige waliofanywa kitoweo cha kulia sima, wali na kadhalika.

Nzige hao waliripotiwa kuonekana kwanza kaunti ya Trans Nzoia kisha wakaanza kuenea wakielekea mlima Elgon na sasa wanapatikana Bungoma.


Licha ya serikali kutoa onyo kwa wakaazi wa magharibi kutowala nzige hao, bado wananchi wanaendelea kujiburudisha kwa mana hiyo iliyojishusha yenyewe kutoka mbinguni.

Utafiti uliofanywa na shirika la International Centre of Insects Psychology and Ecology (ICIPE) hapa nchini Kenya kupitia mtaalamu wake Baldwyn Torto ulieleza manufaa ya kuwala nzige.

Baldwyn Torto anaeleza kuwa nzige hasa wale wa jangwa ( Schistocerca gregaria ) huwa na protini na madini mengine mengi ambayo huimarisha kinga ya mwili wa binadamu, kuzuia saratani na kuvimba kwa viungo vya mwilini.

Kate Kibarah, mwanalishe na daktari humu nchini naye anahimiza kuwa vyakula vya kiasili ambavyo vinaweza vikazuia magonjwa yasiyoambukizwa vipigwe jeki nchini.
Anapongeza utafiti uliofanywa mnamo Mei 13, 2015 ulioongozwa na Baldwyn Torto na kusema kuwa nzige kama lishe wanafaa kutumika na binadamu.

Utafiti huo ulionesha kuwa mimea huwa na madini yaitwayo phytosterols na nzige wanapokula mimea hiyo kisha waliwe na binadamu hujenga afya ya binadamu maradufu!

Imeandikwa na Aggrey Barasa

About Author

1 thought on “Nzige wavamiwa Bungoma

  1. If its true they’re harmless then consumption shouldn’t be an issue. Because they’re here to stay apparently

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *