Noordin Haji awatahadharisha wanaodhulumu wasichana kimapenzi

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji

 Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji amewatahadharisha wanaodhulumu watoto hususan wasichana kimapenzi akisema afisi yake itahakikisha wamechukuliwa hatua kisheria.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa kukinga watoto dhidi ya dhulma za kimapenzi kwa minajili ya fedha katika ukanda wa pwani na shirika la Global Fund pamoja na ujumbe wa kimataifa wa haki IJM, Haji amedokeza afisi yake imebuni sera na taratibu zitakazohakikisha watoto wamelindwa dhidi ya dhulma za kingono.

Kupitia mradi wa ‘ODPP Uadilifu’ data zitakusanywa na kusaidia kugundua mianya inayofaa kuzibwa katika kampeni ya kulinda watoto.

Haji amesifia mradi wa IJM akisema utahamasisha umma kuripoti visa hivyo na kueleza imani yake kuwa mashirika mengine yataungana na IJM katika kampeni hiyo.

Kulingana na Claire Wilkinson anayesimamia idara ya mikakati kwenye shirika la IJM 1 kati ya 4 wanaodhulumiwa ni mtoto, takwimu kutoka shirika hilo zikionyesha kuna takriban waathiriwa 20,000 wa biashara za ng’ono.

Wilkinson amesema wananuia kuimarisha jamii ili kutengeneza mazingira ambapo watoto watalindwa kwa ushirikiano na serikali kuu, idara za haki na washirika.

“Sheria inapotekelezwa,uhalifu hupungua.Tumeokoa waathiriwa 64,000 ndani ya miaka 22 ya oparesheni hii.Tunaazma ya kulinda watoto milioni 21 kote ulimwenguni ifikiapo 2030 dhidi ya dhulma za kingono,’’ akasema Bi Wilkinson.

Bi Mueni Mutisya mkuu wa kitengo cha kulinda watoto na kupambana na uuzaji haramu wa binadamu amesema afisi yake imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na visa vya dhulma kwa watoto huku akieleza upungufu kwa upande wa wananchi kuripoti visa vya biashara ya ngono kwa watoto.

“Tutaimarisha ushirikiano na asasi za serikali pamoja na zile zisizo za serikali kwa lengo la kukomesha dhulma za watoto.Tutazingatia kuimarisha utaratibu wa uwajibikaji,” akasema Bi Mutisya.

Shirika la IJM linanuia kulinda maelfu ya watoto kutoka familia maskini dhidi ya kuingizwa kwenye biashara za ngono, ukanda wa Pwani ukitajwa kuathirika pakubwa na uhalifu huo.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *