Migomo imekosesha vyuo vikuu ladha

Migomo ya mara kwa mara katika vyuo vikuu imevikosesha ladha kabisa. Kila mwaka au muhula angalau mgomo wa wanafunzi wa chuo kikuu huripotiwa. Migomo hiyo hulazimu utawala wa chuo husika kusitisha shughuli zote chuoni.

Wanafunzi hulazimika au hufurushwa kutoka chuoni huku shughuli nzima za kimasomo zikisambaratika. Hali hii husababisha hasara mbalimbali kama zilivyoorodheshwa ifwatavyo:

Kuzidisha muda wa kuwa chuoni.


Muhula unapositishwa, shughuli za kimasomo hulemazwa. Kila likizo ya ghafla inapofwatia mgomo humaanisha kuwa muhula huo utasongeshwa mbele. Hali hiyo hutokea ili kazi ambayo ingefundishwa kwa muhula huo iwe ya muhula unaofwata na kuathiri mihula mingine ya mbeleni.

Likizo inapochukua miezi kadhaa kwa mfano, humeza muhula mzima hivyo kusababisha muda wa wanafunzi kukamilisha masomo yao kuzidi kawaida. Hilo linaweza likasababisha wanafunzi ‘kuzeeka’ wakiwa wangali chuoni.

Kuzidisha gharama kwa wazazi


Wanafunzi wanapozidi kuishi chuoni kwa kipindi kinachozidi kile kilichodhamiriwa, bajeti ya wazazi huathirika. Gharama kama vile kodi, chakula na pesa za matumizi huongezeka vya kutisha. Inamsikitisha sana mzazi kulipia kodi ya mwanawe ambaye haendi darasani, kazi yake ni kujipweteka tu chumbani, kula na kurandaranda mijini.

Wakati mwingine wazazi huwa wamefanya makadirio yao ya muhula namna wanao watakavyoishi wakihudhuria vipindi vya madarasa. Wao hupata ugumu sana kuanza kugharamika zaidi ya kawaida. Vilevile, wanafunzi wanaofurushwa katika mabweni ya ndani ya chuo hulazimika kuitisha nauli kutoka kwa wazazi wao, hiyo ni gharama ya ziada. Wakati mwingine iwapo mgomo wenyewe ulihusisha uharibifu wowote wa mali ya chuo, wanafunzi hulazimika kufidia kwa ada fulani ambayo hulipwa na wazazi wao.

Kuhatarisha maisha


Mara nyingi migomo ya wanafunzi wa vyuoni hudhibitiwa na maafisa wa polisi. Wanapofika kutuliza fujo yenyewe, wanafunzi watundu huonesha kiburi chao kwa kutaka kukabiliana nao. Matokeo ya hali hiyo mbaya huwa baadhi ya wanafunzi kuuawa kwa mapigo mabaya huku wengine wakilemazwa kwa majeraha ya ‘mipini’.

Vilevile baadhi ya wanafunzi hukumbana na hatari za kuvunjika au kuchomwa na vifaa hatari wanapojaribu kutorokea usalama wao. Isitoshe, wanafunzi wenyewe wanaweza wakaumizana wao kwa wao wanapotupa mawe na njiti wakati wa fujo.

Kufukuzwa chuoni


Kama ada, wanafunzi wanaoshukiwa kuwa waanzilishi wa migomo huadhibiwa kwa kosa la uchochezi. Viranja mbalimbali hushutumiwa kwa kutepetea katika uwajibikaji kisha kupewa adhabu ya kufukuzwa chuoni kwa muda. Kwa kweli ni jambo la kutia huzuni machoni pa mzazi hasa wa kimaskini kuona kuwa mwanawe amefurushwa chuoni.

Wengi wa wachochole huwa wamelelea tumaini lao katika wanao wa vyuo vikuu. Kukosa kuwapo chuoni kwa kipindi kirefu kuna athari hasi mno. Mwanafunzi mhusika huwekewa vikwaso vingi na utawala ili viwe vizuizi kwake asiwahi kuhafali chuoni humo; kama njia ya kulipiza kisasi.

Aggrey Barasa

About Author

2 thoughts on “Migomo imekosesha vyuo vikuu ladha

  1. Ni kweli kabisa; lakini kwa upande wangu licha ya changamoto kadhaa zinazoambatana na migomo hii, nakubaliana nalo. Sisi Kama wanafunzi tunastahili kupewa huduma bora na toshelezi…. So bora hiduma.!

    Viva! Viva! Viva

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *