Kifo cha Magufuli kimedhalilisha ‘imani ya mwafrika’

Hayati Dkt John Pombe Magufuli (Picha Kwa Hisani)

Kabla ya kifo cha Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ulimwengu wote ulikuwa umemtambua kama binadamu wa kipekee aliyekiri kutojua maana ya neno ‘corona’. Magufuli hakukubali uwepo wa virusi hatari vya corona hadi baadaye alipoanza kukiri kuwa virusi hivyo vipo; japo ni dhaifu kuliko imani ya watanzania wote.

Rais huyo alisimama tisti kwenye majukwaa akitangaza ushindi wa watanzania dhidi ya virusi hatari vilivyotikisa dunia nzima.Shirika la afya duniani, WHO, lilishtuka! Mataifa makubwa ya ughaibuni yakatikisa vichwa kwa mshangao! Majirani wa Tanzania wakatamani wangekuwa na rais kama yeye.

Mjanja mmoja alisikika akisema kwamba nguvu za kina Kinjeketile Ngwale, Abdala Mpanda na Ngamea walioongoza watanzania kushinda vita vya kati ya mwaka wa 1905 na 1907 dhidi ya wajerumani kwa nguvu-maji zimerudi tena! Vile vita vilivyoitwa ‘majimaji rebellion’.

Aidha, rais Magufuli alijibu mishtuko hiyo kwa kauli kwamba watanzania “wanamwamini Mungu”. Kila aliposikika akisema jukwaani, alitaja nguvu za mwenyezi Mungu katika vita vya watanzania dhidi ya virusi vya corona.

Magufuli hakuonekana kutishika na virusi hivyo vilivyotokea sijui wapi.Watanzania waliendelea na maisha yao kama kawaida bila kujali wala kubali vikwaso vilivyowekwa na shirika la afya duniani.

Mataifa mengine yalipozidi kupima, kurekodi na kutetemekea maafa ya ugonjwa huo waliouita hatari, taifa la Tanzania liliendelea ‘kula bata na kunywa mvinyo’ chini ya mnazi….ufukweni mwa bahari kubwa ya raha na uhuru.

Wakati mmoja Rais wa jamhuri ya Kenya alipotangaza kufungwa kwa baadhi ya shughuli muhimu nchini humo, wakati huo huo ndipo Magufuli wa Tanzania alipokuwa anatangaza uhuru bila wasiwasi wala mshikemshike; mlevi mmoja akasikika akiboboka eti “Magufuli anawapa watanzania uhuru wakati ambapo Uhuru anapiga wakenya makufuli…” alichekesha wapitanjia waliomsikia jioni hiyo.

Baadhi ya wakenya waliruka mitandaoni wakaanza kukashifu marais wa mataifa ya kiafrika kwa kukosa kuiga ‘mfano mzuri’ wa mwenzao. Walitaka marais wengine kuiga imani ya rais Magufuli kuhusu uwepo wa virusi vya ‘kigeni’ katika bara hili lenye watu wenye ‘ngozi ngumu’.

Magufuli alizidi kushikilia msimamo kwamba watanzania wanamwamini Mungu na kwamba hakuna afisa yeyote wa uhamisho katika malango ya taifa lake atakayekubali kuvipa virusi vya corona cheti cha uraia nchini humo. Kwa hivyo, corona haingeweza kuingia Tanzania.

Alisadifu mwaka jana Tanzania ilikuwa inajiandaa kwa uchaguzi mkuu ilhali huo ndio mwaka ambao virusi vya corona vilibisha malango ya dunia. Watanzania waliendelea na shughuli zao za kampeni bila barakoa wala kinga yoyote.

Viwanja vya michezo vilifurika wazalendo kwa maelfu na mamia ya maelfu. Uchaguzi ulifanyika na rais wa watu, chaguo la wengi, kipenzi cha watanzania,Dkt  John Pombe Magufuli akaibuka mshindi kwa kura nyingi sana.

Wakristo walimwona Magufuli kama kiongozi aliyemwamini Mungu zaidi ya mipaka. Walitamani na kuwashurutisha viongozi wao katika nyanja za kisiasa, kidini na kijamii kujaribu kuvaa ngozi ya Magufuli; kiimani.

Juhudi za mashirika mbalimbali ya kimataifa kumshawishi na kumwonya Magufuli kuambatana na tahadhari zilizowekwa dhidi ya maambukizi na maenezi ya virusi vya corona zilikutana na jawabu la “sisi watanzania tunamwamini Mungu; tutakunywa maji ya ndimu, saumu na tangawizi kisha tufunge kwa kupiga mazoezi hatali….”

Sifa za rais huyo ambaye kwa sasa alimrudia muumba zilitamba na kutamalaki kotekote. Magufuli alikuwa picha kamili ya mwafrika tisti katika maneno na vitendo vyake. Magwiji katika mataifa ya kiafrika walijitokeza kumpongeza kwa udhabiti wake na uzalendo kwa tamaduni za kiafrika.

Mlumbi mkenya,Profesa  PLO Lumumba, alibuni neno ‘Magufulification of Africa’ akirejelea ubingwa wa Dkt John Pombe Magufuli na kuulinganisha na uhitaji wa nguvu dhabiti za kimaendeleo barani Afrika. Gazeti moja la Afrika Kusini lilinukuu maneno ya Rais huyo na kusifia utendakazi wake katika taifa la Tanzania.

Mwimbaji wa kitanzania ‘Harmonize’ alitunga wimbo mtamu zaidi akisifia nguvu za Magufuli katika njia mbalimbali. Sifa za daktari rais mchapakazi zilitanda kotekote. Imani ya kiafrika ilijengwa na kusimama tisti katika taifa la Tanzania. Wengi walitamani sana rais John Pombe Magufuli aishi miaka mingi ili aendeleze ujivuniaji wa uafrika miongoni mwa waafrika.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *