Chanjo ni salama, Serikali yasema

Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwenye wizara ya afya(kwenye kiti) Patrick Amoth akipokezwa chanjo ya Astrazeneca na muhuduma wa afya Picha kutoka Twita Wizara ya Afya

Serikali ya Kenya imewahakikishia  wakenya kuwa chanjo ya Astrazeneca iliyowasili nchini Jumatano Machi 3,2021 chini ya mpango wa COVAX kutoka umoja wa mataifa UN ni salama kwa afya.

Kaimu mkurugenzi kwenye wizara ya Afya Patrick Amoth ameeleza kuwa chanjo hiyo imefanyiwa majaribio na utafiti wa kutosha kabla ya kuidhinishwa, hivyo basi wakenya wasiwe na hofu kuchukua chanjo hiyo.

Amoth ambaye amekuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo katika hospitali kuu ya Kenyatta ameelezea matumaini yake kuwa maisha itarudi kama kawaida baada ya asilimia kubwa ya wakenya kuchanjwa.Vilevile amedokeza kuwa chanjo hizo zitapokezwa kwenye kaunti kuanzia wiki ijayo.

Kauli ya Amoth imesisitizwa na Mwelekezi wa umoja wa mataifa nchini Kenya Stephen Jackson ambaye ameipongeza Kenya kwa hatua hiyo kubwa kwa vita dhidi ya janga la Korona.

Jackson amewarai wakenya kuzidi kuzingatia sheria zilizowekwa na wizara ya afya kukabili Korona hata baada ya kupokea chanjo hiyo  na vilevile kupuzilia mbali habari potovu zinazoenezwa mtandaoni kuhusu virusi vya korona na chanjo ya Astrazeneca na badala yake kuamini wizara ya afya.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati ya dharura ya kushughulikia janga la korona Githingi Gitahi wahudumu wa afya watapokea mafunzo ya namna ya kupokeza chanjo hiyo ili kuhakikisha shughuli hiyo imefanyika kwa utaratibu unaohitajika.

Ameongezea kuwa serikali ya Kenya imejitolea kuhakikisha kuwa kila mkenya anapokea chanjo hiyo.

Kamati hiyo imebuni kamati zingine zitakazosaidia kuhakikisha kuwa shughuli za kupokeza chanjo nchini imeenda shwari kama ilivyopangwa.

Kamati ya data itakusanya data ya wakenya waliopokea chanjo hiyo huku kamati ya mipango na uratibu itahakikisha kuwa mpango wa serikali imetimizwa kwenye kaunti hadi vijijini na pia inalingana na malengo ya mashirika yaliyosaidia shughuli hiyo.kamati zingine ni ile ya kudhibiti na kuhakikisha usalama wa chanjo hiyo pamoja na kamati ya ununuzi wa vifaa.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *